Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)

Elimu Haki Wajibu

MAJAJI WA TANZANIA NA CANADA KUBADILISHANA UZOEFU WA MATUMIZI YA DNA KWENYE MIFUMO YA HAKI JINAI

Imewekwa: 26 September, 2025
MAJAJI WA TANZANIA NA CANADA KUBADILISHANA UZOEFU WA MATUMIZI YA DNA KWENYE MIFUMO YA HAKI JINAI

Majaji wa Mahakama ya Tanzania na Canada wanatarajia kushirikiana na kubadilishana uzoezi katika matumizi ya vinasaba (DNA) kama nyanzo vya kisayansi ya kuthibitisha ushahidi Mahakamani.

Aidha hatua hii inalenga  kukuza na kuimarisha mifumo ya haki jinai hapa nchini hususani kipindi hiki cha maendeleo ya teknolojia katika utoaji wa haki.

Pia kupitia mpango huo, Majaji wa Tanzania watapata fursa ya kwenda nchini Canada kwa ajili ya kujifunza kivitendo namna Mahakama za nchi hiyo zinavyotumia ushahidi wa DNA katika kusikiliza na kuamua mashauri ya jinai.

Vile vile Majaji hao pamoja na Maafisa wengine wa Mahakama ya Tanzania wanatarajiwa kupatiwa mafunzo maalumu kuhusu matumzi hayo ya DNA katika kuamua mashauri ya jinai, ambayo yatafanyika hapa nchini siku za usoni mara baada ya mchakato wa mafunzo hayo kukamilika.

Mazungumzo ya awali kuhusu mchakato huo yalifanyika Septemba 25, 2025 Chuoni Lushoto baina ya Maafisa wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) pamoja  na Afisa kutoka Ubalozi wa Canada hapa nchini Tanzania.

Maafisa wa IJA waliyoshiriki majadiliano hayo ni Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo, Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama na Elimu Endelevu IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda, Mhe. Patrick Lipiki Katibu wa Mkuu wa Chuo na Mratibu wa Mafunzo na kwa upande wa Ubalozi wa Canada hapa nchini ni  Mshauri wa Siasa, Uchumi na Utamaduni Bw. Eric Kendrick.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Dkt. Kihwelo amesema kuwa kubadilishana uzoefu ni muhimu katika mifumo ya Mahakama, akibainisha kuwa hatua hiyo itawasaidia Majaji na wadau wa haki kuboresha namna ya kutumia DNA katika utoaji haki.

Kwa upande wake, Bw. Kendrick alieleza kufurahishwa kwake na jitihada zinazofanywa na IJA katika kukuza uwezo wa Maafisa wa Mahakama katika eneo la utoaji haki.

Katika hatua nyingine, Bw. Kendrick amesifu miundombinu mbalimbali iliyopo Chuoni hapa ambayo inatoa nafasi ya utoaji wa mafunzo ya Kimahakama na yale ya Astashahada na Stashahada ya Sheria.