JAJI MWANABARAKA AFUNGUA MAFUNZO YA KUEPUKA KUTONESHA MAJERAHA KWA WAATHIRIKA WA UKATILI WA KINGONO

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania – Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke Dar es Salaam Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa amefungua Mafunzo ya awamu ya tatu ya Kuepuka Kutonesha Majeraha kwa Waathirika wa Ukatili wa Kingono (Avoiding Re-traumatization to sexual abuse victims) ambayo yanatolewa kwa Mahakimu Wakazi, Waendesha Mashtaka, na Maafisa Ustawi wa Jamii
Amefungua mafunzo hayo tarehe 14/04/2025 ambayo yatafanyika hadi tarehe 16/04/2025 katika kituo hicho Jumuishi.
Mafunzo hayo yameandaliwa na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Irish Rule of Law International (IRLI) kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mhe. Jaji Mwanabaraka amesisitiza umuhimu wa kutumia lugha yenye huruma, staha, uweledi mkubwa, pamoja na kujenga mazingira rafiki ya kimahakama kwa waathirika wa ukatili huo.
Vilevile, amehimiza washiriki kuwa makini na mbinu wanazotumia katika kushughulikia mashahidi walio katika mazingira magumu ili wasiwajengee hali ya woga au kukumbuka majeraha yao ya awali.
Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama IJA ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mkuu Mhe Dkt. Patricia Kisinda na Mratibu wa Mafunzo IJA ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mhe. Husna Rweikiza. Hawa wataongoza washiriki kupitia mijadala na mafunzo ya vitendo yenye kuhusisha uzoefu wa kiutendaji katika masuala hayo ya ukatili wa kingono.
Aidha mafunzo hayo ambayo yameshafanyika wilayani Lushoto na Dodoma yamelenga kuwajengea uwezo washiriki katika kushughulikia mashauri ya ukatili wa kijinsia kwa kuzingatia athari za kiakili na kihisia kwa waathirika, sambamba na kuheshimu haki za watuhumiwa.
Mafunzo haya yamekuwa sehemu ya jitihada za Mahakama ya Tanzania—chini ya uongozi wa wa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma za kuboresha mifumo ya utoaji haki ili iwe jumuishi, yenye huruma, na inayo wajali wahitaji mbalimbali wakiwemo waathirika wa ukatili wa kijinsia.