Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)

Elimu Haki Wajibu

GIZ NA KLABU ZA WANACHUO IJA WAJADILI MIKAKATI YA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA LUSHOTO

Imewekwa: 10 April, 2025
GIZ NA KLABU ZA WANACHUO IJA WAJADILI MIKAKATI YA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA LUSHOTO

Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) limekutana na klabu mbalimbali za Wanachuo wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ili kujadili masuala ya kufanya ndani ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

Kikao hicho cha majadiliano hayo kimefanyika leo tarehe 10/04/2025 hapa Chuoni Lushoto na kuhudhuriwa na watumishi wa Chuo, viongozi na wanachama wa klabu hizo.

Majadiliano hayo yamelenga kupambana na matukio ya ukatili wa kijinsia ndani ya wilaya ya Lushoto katika kipindi hicho cha siku 16.

Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ni kampeni ya Kimataifa ya  kupinga ukatili dhidi ya wanawake na hufanyika kuanzia Novemba 25 mpaka Desemba 10 ya kila mwaka.

Kabla ya majadiliano hayo, kiongozi wa mradi wa ukuzaji wa Utawala wa Sheria na Mahakama Barani Afrika (ProLA) Bw. Muhamet Brahimi pamoja na Afisa Mawasiliano na utetezi wa mradi wa upatikanaji haki sawa kwa wanawake na watoto (SAFE) Bi. Agness John waliwapitisha wanachama hao juu ya miradi mbalimbali inayoendeshwa na GIZ hapa nchini ikiwemo ya kushirikiana na wanafunzi wa baadhi ya vyuo katika kukuza uelewa wa kisheria kwa jamii na kupambana na ukatili wa kijinsia.

Wanachama hao ni wa Klabu za Mazingira, Taaluma, Mahakama, Rushwa (PCCB Club), Mazoezi (Jogging) na inayojihusisha na masuala ya kijinsia (HeforShe)

GIZ ni miongoni mwa wadau wakubwa wa IJA ambapo imewezesha kuendeshwa kwa mafunzo mbalimbali yakiwemo ya maafisa wa Mahakama.

Pia GIZ ilishirikiana na IJA katika zoezi la utoaji wa elimu na msaada wa kisheria kwa wakazi wa kata za Mbaramo na Mnazi katika wilaya ya Lushoto Septemba mwaka jana.