Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)

Elimu Haki Wajibu

IJA YATOA TUZO KWA VYOMBO VYA HABARI KUTAMBUA MCHANGO WAO KATIKA MAFANIKIO YA CHUO

Imewekwa: 20 July, 2026
IJA YATOA TUZO KWA VYOMBO VYA HABARI KUTAMBUA MCHANGO WAO KATIKA MAFANIKIO YA CHUO

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kimetoa tuzo za shukrani kwa baadhi ya vyombo vya habari kwa kutambua mchango wao mkubwa katika kuhabarisha umma kuhusu shughuli, mafanikio na huduma zinazotolewa na Chuo.

Vyombo vya habari vilivyotunukiwa tuzo hizo ni Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Channel 10 na Gazeti la The Citzien, katika hafla iliyofanyika leo Julai 20, 2026 jijini Dar es Salaam.

Tuzo hizo zimekabidhiwa na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani,  Mhe. Dkt. Mary C. Levira. Waliopokea tuzo kwa niaba ya vyombo vyao ni Mkurugenzi wa Huduma za Televisheni wa TBC, Bi. Happiness Ngasala, Mhariri Mkuu wa Africa Media Group,  Bw. Ezekiel Mwambopo, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Africa Media Group; pamoja na Mhariri Mtendaji Mkuu anayesimamia Idara ya Maudhui wa Mwananchi Communications Limited, Bw. Mpoki Thomson.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Dkt. Levira alisema tuzo hizo ni ishara ya heshima, shukrani na utambuzi wa mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika kujenga taswira chanya ya Chuo na kuimarisha uelewa wa umma kuhusu shughuli zake.

“Tuzo tunazokabidhi leo si zawadi ya kawaida. Ni ishara ya heshima, shukrani na utambuzi wa mchango wenu katika kujenga taswira chanya ya Chuo. Ni uthibitisho kwamba tunathamini ushirikiano mnaokipatia Chuo chetu katika sekta ya habari na mawasiliano,” alisema.

Ameongeza kuwa IJA itaendelea kushirikiana kwa karibu na vyombo vya habari kwa kuhakikisha vinapata taarifa kwa wakati, kwa usahihi ili viendelee kutekeleza wajibu wao wa kuhabarisha umma.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo amesema vyombo vya habari ni wadau muhimu katika kufikisha kwa wananchi habari, mafanikio ya Chuo katika kuendeleza sekta ya sheria na utoaji wa haki nchini.

Amesema bila ushirikiano wa vyombo vya habari, wananchi wengi wasingeweza kufahamu kazi inayofanywa na IJA katika kuandaa wataalamu wa sheria, kujenga uwezo wa watumishi wa Mahakama na wadau wengine wa sekta ya sheria.

Nao wawakilishi wa vyombo hivyo wameishukuru IJA kwa kutambua mchango wao na kuahidi kuendelea kushirikiana na Chuo katika kuuhabarisha umma kuhusu shughuli, mafanikio na maendeleo yake.