MAELEZO MAFUPI YA MWENYEKITI WA BARAZA KATIKA HAFLA FUPI YA KUMUAGA JAJI MKUU MSTAAFU MHESHIMIWA MOHAMED CHANDE OTHMAN CHUONI LUSHOTO TAREHE 19/08/2017

Mhe. Mgeni Rasmi, Mhe. Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania;

Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Jaji Mohamed Chande Othman;

Mhe. Jaji Aishiel Sumari, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi;

Mhe. Jaji Iman Aboud, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga;

Mhe. Jaji Dkt. Paul F. Kihwelo, Mkuu wa Chuo na Katibu wa Baraza la Uongozi wa Chuo

Mhe. Jaji Amour Khamis, Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Tanga;

Mhe. Jaji Dkt. Benhajj Masoud, Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Tanga;

Mhe. Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu wa Mahakama;

Mhe. Katarina Revocati, Msajili Mkuu;

Mhe. Jaji Emilian Mushi; Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu;

Wahe. Wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Chuo;

Mhe. Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga

Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Lushoto;

Mhe. Mkurugenzi wa Wilaya ya Lushoto;

Mhe. Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Wilaya ya Lushoto;

Mhe. Mwenyekiti wa Kitongoji cha Dochi;

Wawakilishi wa watumishi wa Chuo;

Wageni waalikwa, mabibi na mabwana.

Habari za asubuhi,

Awali ya yote napenda kutumia fursa hii adhimu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kukutana hapa siku hii ya leo kwa minajili ya kumpongeza, kumshukuru na kumuaga Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Jaji Mohamed Chande Othman kwanza kwa kipindi alichokuwa Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hiki, na kwa mchango wako kwa Chuo katika kipindi ulichokuwa unaongoza muhimili muhimu katika utoaji haki nchini, Mahakama ya Tanzania.

Mhe. Mgeni Rasmi, kwa namna ya pekee nachukua fursa hii kukushukuru wewe binafsi kwa kukubali mwaliko wa kuwa mgeni rasmi na kujumuika nasi katika hafla hii fupi ya leo kumpongeza na kumuaga Mhe. Jaji Mohamed Chande Othman.

Mhe. Mgeni Rasmi, siku hii ya leo ni siku muhimu sana na hatuna budi kumpongeza na kumshukuru Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Jaji Mohamed Chande Othman kwa mambo mengi aliyoyafanya katika kukiendeleza Chuo chetu katika kutimiza Dira na Dhamira ya kuanzishwa kwake.

Mhe. Mgeni Rasmi, tunapenda kukufahamisha kwamba Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu ametoa mchango mkubwa sana katika kukiendeleza Chuo chetu kuanzia mwaka 2010 mpaka mwaka, 2012 ulipoteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Pili wa Baraza la Uongozi wa Chuo baada ya Mhe. Balozi Paul Rupia aliyekuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Baraza kumaliza muda wake. Kwa sababu ya muda sitaweza kubainisha yote aliyoyafanya katika kuhakikisha Chuo kinatimiza malengo yake. Pengine ni muhimu kwangu niainishe mambo muhimu machache ambayo Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohamed Chande Othman atakumbukwa nayo hapa chuoni:-

Mhe. Mgeni Rasmi, katika kipindi cha kuanzia tarehe 01/09/2014 hadi 19/09/2014 kwa maelekezo ya Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu kwa mara ya kwanza Chuo kilitoa mafunzo elekezi kwa muda wa majuma matatu mfululizo kwa majaji wapya 20 wa Mahakama Kuu ya Tanzania walioteuliwa na Rais wa Jamhuri yaMuungano wa Tanzania kabla ya kuanza kazi.

Aidha, mafunzo ya aina hiyo yaliendelea kutolewa tena mwaka 2015 kwa Majaji wengine 14 wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuanzia tarehe 21/08/2015 hadi 11/09/2015. Hayo yote yalikuwa ni katika kuhakikisha kwamba kutoa mafunzo elekezi na endelevu yanatolewa kwa waheshimiwa majaji hilo likiwa ni miongoni mwa majukumu ya msingi ya Chuo.

Vile vile mnamo mwezi Julai, 2016 Chuo kwa maelekezo ya Mheshimiwa Jaji Mkuu Mstaafu kiliendesha mafunzo elekezi kwa waheshimiwa majaji walioteuliwa na Mheshimiwa Jaji Mkuu kwa ajili ya kuendesha mashauri katika Mahakama Kuu Kitengo cha Rushwa na Makosa ya Uhujumu Uchumi.

Ni matumaini yetu kwamba Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Uongozi wa Chuo itaendeleza jukumu hili la kutoa mafunzo elekezi kwa majaji wapya punde wanapoteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhe. Mgeni Rasmi, mbali na mafunzo ya Wahe. Majaji wapya wa Mahakama Kuu, Chuo kiliratibu utoaji wa mafunzo mbalimbali kwa waheshimiwa Wasajili, Mahakimu na watumishi wote wa kada za uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Juhudi zote hizi alizifanya Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu ili kukifanya Chuo kuwa kitovu cha utoaji wa mafunzo elekezi na endelevu kwa watumishi wote wa Mahakama kwa kushirikiana na Kitengo cha mafunzo cha mahakama.

Mhe. Mgeni Rasmi, katika mradi wa Benki ya Dunia unaotekelezwa na Mahakama ya Tanzania ambaoumelenga kwenye uboreshaji wa huduma za Mahakama na jinsi ya kusogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi, mheshimiwa Jaji Mkuu Mstaafu akiwa kiongozi wa Mahakama, alihakikisha Chuo ni sehemu ya mradi huo kwa kupewa jukumu la kutoa mafunzo kwa watumishi wa kada zote za Mahakama ikiwemo kada ya juu kabisa ya Majaji wa Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu, lengo likiwa ni pamoja na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama na kujenga weledi utakaorahisisha upatikanaji wa haki, kuboresha utawala wa Mahakama, kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama na ushirikishwaji wa wadau katika kuboresha huduma za Mahakama.

Mhe. Mgeni Rasmi, napenda kutoa taarifa rasmi kuwa mpaka leo hii, Chuo kimeshiriki katika kuendesha mafunzo mbalimbali kwa kipindi cha Desemba, 2016 hadi Juni, 2017 yaliyoratibiwa na Mahakama pamoja na Chuo kwa ufadhili wa Benki ya Dunia. Majaji na watumishi wa kada mbalimbali za Mahakama wakiwemo Wasajili, Watendaji, Mahakimu, Maafisa Tawala, Maafisa Utumishi, Makarani, Makatibu Mahsusi, Madereva na wahudumu wameshiriki katika mafunzo yaliyoandaliwa na Chuo kwa kushirikiana na wawezeshaji mbalimbali.

Mhe. Mgeni Rasmi, napenda pia kukufahamisha kwamba Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu kwa lengo la kuhakikisha kwamba wanaijengea uwezo wa Raslimali watu Kurugenzi ya Mafunzo Endelevu ya Kimahakama inayoratibu na kuendesha mafunzo ya watumishi wa Mahakama wa ngazi zote, alichukua hatua ya kuhamishia Mahakimu Wakazi Waandamizi watatu katika Kurugenzi hii ili wawe waratibu wa Mafunzo hayo kuanzia tarehe 13 Mei, 2016.

Mhe. Mgeni Rasmi, Jaji Mkuu Mstaafu alihakikisha pia anaendeleza mahusiano mazuri yaliyoanzishwa kati ya Chuo na Chama cha Majaji Wanawake Tanzania. Katika kipindi chake cha uongozi, Chama cha Majaji Wanawake Tanzania siyo tu kilitoa mafunzo kwa wanajumuiya ya Chuo, pia kilitoa fursa ya wakufunzi wawili kushirikiana nao katika kuandaa machapisho mnamo mwaka 2014 na mwaka 2016. Wakufunzi hao walishirikiana na Chama hicho katika uandaaji wa Vitini vinavyohusu mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto.

Mhe. Mgeni Rasmi, katika uzinduzi wa kitini cha mwaka 2016, ilizinduliwa pia kampeni ya usawa wa kijinsia ijulikanayo kwa lugha ya kigeni He for She. Chuo katika kuendeleza kampeni hiyo kimeunda klabu ambayo ina wanachama wapatao 60. Miongoni mwa malengo ya klabu hiyo ni kuleta usawa wa jinsia na kupinga unyanyasaji kwa makundi tete ya jamii wakiwemo wanawake na watoto.

Mhe. Mgeni Rasmi, Jaji Mkuu Mstaafu pia alinipa ushirikiano wa kutosha katika utatuzi wa changamoto na kunipa maoni kila nilipopata fursa ya kupeleka changamoto hizo ofisini kwake, tulijadiliana kwa uwazi na kufikia muafaka kwa mustakabali wa Chuo. Ni matumaini yangu kuwa tutaendelea kupata ushirikiano huo katika ofisi yako.

Mhe. Mgeni Rasmi, klabu hiyo imekuwa ni chachu ya ushiriki wa uelimishaji kwa wanachuo hasa kwa wanachama wa klabu hiyo. Mfano kwa mwaka huu klabu imeweza kushiriki vema katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa...