HOTUBA YA MGENI RASMI JAJI IBRAHIM HAMIS JUMA, KAIMU JAJI MKUU KATIKA HAFLA FUPI YA KUMUAGA JAJI MKUU MSTAAFU MHE. MOHAMED CHANDE OTHMAN CHUONI LUSHOTO

TAREHE 19/08/2017

Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Jaji Mohamed Chande Othman;

Mhe. Jaji John Mrosso, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Baraza;

Mhe. Jaji Aishiel Sumari, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi;

Mhe. Jaji Iman Aboud, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga;

Mhe. Jaji Dkt. Paul F. Kihwelo, Mkuu wa Chuo na Katibu wa Baraza la Uongozi wa Chuo

Mhe. Jaji Amour Khamis, Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Tanga;

Mhe. Jaji Dkt. Benhajj Masoud, Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Tanga;

Mhe. Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu wa Mahakama;

Mhe. Katarina Revocati, Msajili Mkuu;

Mhe. Jaji Emilian Mushi; Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu;

Wahe. Wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Chuo;

Mhe. Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga

Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Lushoto;

Mhe. Mkurugenzi wa Wilaya ya Lushoto;

Mhe. Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Wilaya ya Lushoto;

Mhe. Mwenyekiti wa Kitongoji cha Dochi;

Wawakilishi wa watumishi wa Chuo;

Wageni waalikwa, mabibi na mabwana.

Awali ya yote nami nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuweka hai na kutukutanisha katika tukio hili muhimu na la kihistoria kwa Baraza la Uongozi wa Chuo.

Naomba kuwashukuru sana kwa kunialika kuwa mgeni rasmi katika hafla hii ambayo imenipa fursa ya kukitembelea Chuo hiki kwa mara ya kwanza kama Kaimu Jaji Mkuu. Kwa hakika hii ni heshima kubwa mliyonipa ambayo ni fursa nyingine kwangu ya kukutana na wajumbe wa Baraza la Chuo, waheshimiwa majaji na viongozi wa Chuo chetu. Pia, nawashukuru kwa mapokezi mazuri niliyoyapata tangu nilipowasili hapa jana.

Ni Wazo Jema sana kutenga siku Maalum ya kumpongeza Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu:

Mhe. Mwenyekiti na wajumbe wa Baraza, naomba niwapongeze kwa dhati na kuwashukuru kwa wazo na hatimaye kufanikisha hafla ya kumpongeza Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman kwa kutambua mchango wake wa hali na mali katika kukiendeleza chuo chetu hiki. Pia; niwapongeze wale wote waliohusika kwa namna moja au nyingine katika maandalizi ya hafla hii fupi ya kumpongeza na kumuaga Jaji Mkuu Mstaafu.

Haikuwa kazi nyepesi kuamua ni mambo gani niyazungumze kati ya mengi ambayo Mhe. Chande amefanikisha kwa manufaa ya Chuo chetu. Nikaona niwe kama Wataalamu wa Uchumi, ambao hutumia maneno ya kilatini: Ceteris paribus or caeteris paribus (other things equal)—Mambo yote yakibaki sawa. Kwa hiyo, nikaamua kukata kipande tu cha MAISHA YAKE na kujiuliza:

1.Zama hizo Mahakama ya Tanzania ilikuwa inapitia Maboresho/Mabadiliko gani

2.Mhe. Chande alitumiaje Uongozi wake

3.Ameiweka wapi Mahakama na Chuo, na ametoa msukumo gani ambao tunao?

4.Baada ya kumaliza kipindi cha uongozi wake, ni Namna gani, Aura, Personality, Ushawishi wake utaisaidia kusukuma gurudumu la maendeleo/maboresho ya Chuo na Mahakama.

Mhe. Mwenyekiti na wajumbe wa Baraza, Chuo cha Uongozi wa Mahakama ni moja ya taasisi nyeti na muhimu sana ndani ya Mahakama ya Tanzania. Ni taasisi ambayo imepewa jukumu kubwa na zito la kuwanoa na kuwajengea weledi watumishi wa kada zote za Mahakama ya Tanzania.

Uwepo wa Chuo hiki ni chachu ya utoaji haki kwa wote na kwa wakati. Hivyo, napenda kumpongeza Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu kwa kuziimarisha misingi mizuri ya kukitumia vema chuo chetu kama kitovu cha kutoa mafunzo elekezi na mafunzo endelevu kwa watumishi wa ngazi zote wa Mahakama na ili waiwezeshe Mahakama kufikia lengo la DIRA ya Haki sawa kwa wote na kwa wakati na DHIMA ya Mahakama ya Tanzaia (Kutoa haki katika mazingira ya haki, usawa, uwazi na kwa kuzingatia maadili ya utendaji kazi kama inavyotarajiwa na Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa mwaka 2015/16 – 2019/20.

Mchango wa Mhe. Chande Kuinua nafasi ya Chuo

Mhe. Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza, tutamkumbuka sana Mhe. Chande kwa kusimamia utayarishwaji wa Mpango Mkakati wa Miaka 5 (2015-2020) wa Mahakama unaolenga kuboresha huduma za Kimahakama nchini ikiongozwa na DIRA YA HAKI KWA WOTE NA KWA WAKATI. Mpango huu ambao unaotoa mwelekeo wa Mahakama, umetoa nafasi muhimu sana kwa Kwa Chuo cha Uongozi wa Mahakama. Wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati mwaka jana (2016), Mhe. Chande alitambua nafasi MPYA ya Chuo chetu katika MABORESHO YA MAHAKAMA kwa kutamka nia ya:

“Kuimarisha Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ili kiwe chenye hadhi na kitoe mafunzo kwa maofisa wa Mahakama na wadau wengine.”

Mhe. Chande aliamini kuwa haitoshi kuwa na MPANGO MKAKATI kama mpango huo unabaki vitabuni bila ya kutekelezwa kwa Vitendo. Kwa bahati nzuri, matarajio makubwa ya Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Chande kuwa Chuo hiki kiwe sehemu muhimu ya Mpango Mkakati, tayari yanatekelezwa kwa vitendo sasa hivi chini ya mradi wa maboresho unaofadhiliwa na Benki ya Dunia. Uongozi wa Chuo, kwa kushirikiana na Timu Kutoka Kitengo Cha Mafunzo Cha Mahakama, imetayarisha RASIMU YA MPANGO WA MAFUNZO WA MAHAKAMA WA MUDA MFUPI (wa Mwaka mmoja—2017/2018). Mpango huu wa mafunzo ambao ni shirikishi, umeainisha malengo ya mafunzo, mahitaji, mikakati ya utekelezaji na mitaala ambayo ikitekelezwa itakuwa ni kwa manufaa kwa mahakama kwa ujumla.

KWA KUINUA NAFASI YA CHUO kuwa katika nafasi inayotegemewa na Mahakama, ni KIRITHI KIKUBWA CHA Mhe. Chande (His lasting legacy)

Nafasi ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Kuendeleza Legacy (Kirithi) ya Viongozi waliotangulia

Hapa Tanzania, tuna utamaduni mzuri wa kuwarudia viongozi wetu waliomaliza vipindi vyao kwa ajili ya ajili ya kupata ushauri, na wengine huita kuchota busara za uzoefu wao:

“African wisdom stresses that the community of human has three facets, those who went before us, those who are alive here and now and those who are yet to come”— Justice Christopher Weeramantry].

Dhana ya Siku ya leo haina lengo la kumuaga na kumsahau Mhe. Chande bali kumtayarisha kuwa awe tayari kuendelea kutoa ushauri na busara zake. Mimi nadhani leo ni siku maalum ya Chuo kutafakari kipindi chake cha uongozi na kurejea mafanikio yake na fikra zake kuhusu Chuo na Mahakama, na kuzitumia katika maendeleo ya Chuo na Mahakama. Nitatoa mifano ya mambo kadhaa yaliyojitokeza wakati wa uongozi wa Mhe. Jaji Chande na ubunifu unaotakiwa kufanywa na Chuo ili kuendeleza legacy (kirithi) cha kipindi hicho.

Katika kipindi cha miaka sita na zaidi, kuanzia 28 December 2010 hadi 18 January 2017 Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Chande alikuwa Jaji Mkuu na kuna mambo mengi ambayo aliyatekeleza au alisimamia utekelezwaji. Haya ni mambo ambayo Chuo cha Uongozi wa Mahakama kinaweza kuyafanyia ubunifu kwa faida ya kuyaendeleza.

(i)Kuwa na Mafunzo Endelevu kwa Kada ya

Watendaji

Juhudi za Maboresho ya Sekta ya Sheria ni ya muda mrefu. Mwaka 2011 baada ya majadiliano ya muda mrefu kuanzia Tume ya Msekwa (Judicial Review Commission, 1977) na Tume ya Bomani (Legal Task Force Report, 1993). Bunge hatimaye lilitunga SHERIA YA UENDESHAJI WA MAHAKAMA, NA. 4 YA 2011 wakati wa uongozi wa Mhe. Chande ambaye anafahamu sana majadiliano yaliyosukuma kutungwa kwa Sheria hii, nini ili...