HOTUBA YA KUFUNGA MAFUNZO YA UTUNZAJI WA KISASA WA KUMBUKUMBU KIELEKTRONIKI KWA WATUNZA KUMBUKUMBU WASAIDIZI WA MAHAKAMA YA TANZANIA YALIYOFANYIKA CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA LUSHOTO KUANZIA TAREHE 3/1/2017 – 13/1/2017

 • -Mheshimiwa Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri;
 • -Mheshimiwa Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo - Mahakama ya Tanzania;
 • -Ndugu Wakufunzi,
 • -Waandaji wa Mafunzo kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto;
 • -Mwenyekiti wa Washiriki;
 • -Ndugu Washiriki;
 • -Mabibi na Mabwana.

Habari za Mchana.

Napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujaalia afya njema kwa kipindi cha siku kumi ambazo mmekuwa hapa chuoni kuhudhuria mafunzo ambayo ni chachu na msingi wa utendaji kazi bora katika fani yenu ya Utunzaji wa Kumbukumbu.

Nichukue fursa hii pia kuushukuru Uongozi wa Chuo kwa kuniteua kufunga mafunzo haya nikiwa Mwakilishi wa Serikali Wilayani Lushoto.

Aidha, nachukua fursa hii tunapokamilisha mafunzo haya kuwashukuru kwa dhati timu ya wawezeshaji mahiri kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Taasisi ya Mafunzo ya Sheria Tanzania, na Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa.

Niishukuru pia Sekretarieti ya Mafunzo ya Kimahakama iliyopo hapa chuoni kwa kufanikisha mafunzo haya.

Ndugu Washiriki,

Natambua kuwa mafunzo haya yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama wa Mwaka 2015/16 – 2019/20 wenye lengo la Kurejesha Imani ya Jamii na Ushirikishwaji wa Wadau katika Shughuli za Mahakama.

Aidha, nachukua fursa hii kuwashukuru Benki ya Dunia ambao wamefadhili mafunzo haya kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma uliotukuka wenye viwango na weledi chini ya Dira ya Haki Sawa kwa Wote na kwa Wakati.

Ndugu Washiriki,

Nimeelezwa kuwa washiriki wa mafunzo haya ni Makarani Wasaidizi na Wataalamu wa TEHAMA na kuwa mafunzo haya ni chachu ya kupata watumishi walioiva ambao wataleta ufanisi katika utendaji kazi mara baada ya mafunzo hayo.

Ndugu Washiriki,

Naomba niwasisitize washiriki wote kuwa mafunzo haya mliyoyapata ya Utunzaji wa Kisasa wa Kumbukumbu Kielektroniki mnawajibu mkubwa wa kufanyia kazi mafunzo hayo kivitendo huko muendako na muendelee kuwa na nidhamu na uadilifu ili kurejesha imani ya jamii dhidi ya Mahakama.Hivyo basi, naomba muelewe kuwa dhamana mliyopewa ni kubwa sana kwa mustakabali wa Mahakama ya Tanzania na Taifa kwa ujumla.

Ndugu Washiriki,

Naomba nibainishe Matarajio ya Mahakama Baada ya Mafunzo haya:

 • 1.Kuimarisha na kuboresha kazi ya Utunzaji wa Kisasa wa Kumbukumbu Kielektroniki kwa lengo la kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia;
 • 2.Kuongezeka kwa ubora wa uandaaji wa taarifa za takwimu kwa njia ya Kieletroniki ambazo huwa mnaziandaa kila mwezi kwa kushirikiana na watumishi wenzenu;
 • 3.Elimu na ujuzi mlioupata katika mafunzo hayo mkawafundishe na wenzenu ambao hawakubahatika kuhudhuria mafunzo haya; na
 • 4.Mkawe mabalozi wa mabadiliko ya kiutendaji yenye kuleta matokeo chanya ili kuongeza kiwango cha kuridhika kwa wadau wa huduma za Mahakama.

Ndugu Washiriki,

Naomba nichukue fursa hii kuwapongeza Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Mahakama ya Tanzania kwa kuzidi kuwanoa watumishi wa mahakama kwa lengo la kuimamrisha taaluma ya kisheria, kiutawala na ujuzi kwa watumishi wa ngazi zote wakiwemo Majaji, Wasajili, Manaibu Wasajili, Mahakimu, Watawala, Makarani na Watumishi wengine.

Ndugu Washiriki;

Nichukue fursa hii adhimu tunapohitimisha mafunzo haya ya siku kumi kuwashukuru tena kwa dhati timu ya wakufunzi, sekretarieti ya mafunzo ya kimahakama iliyopo hapa chuoni kwa kufanikisha mafunzo haya.

Aidha, niwatakie safari njema wakufunzi na washiriki wote katika safari ya kurejea katika vituo vyenu vya kazi.Napenda kutamka kwamba Mafunzo haya ya siku kumi yamefungwa rasmi.

Ahsanteni sana.

Mhe. January Lugangika

MKUU WA WILAYA – LUSHOTO

13/01/2017