MAELEZO YA MKUU WA CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA LUSHOTO KATIKA MAHAFALI YA 16 YA CHUO, TAREHE 02 DESEMBA, 2016

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb), Waziri wa Katiba na Sheria;

Mheshimiwa Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, John A. Mroso Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo;

Mheshimiwa Jaji Aishieri Sumari, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Moshi;

Mheshimiwa Jaji Imani Aboud, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Tanga;

Mheshimiwa Professor Sifuni Mchome, Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria;

Mheshimiwa Emilian E. Mushi, Jaji Mstaafu Mahakama Kuu ya Tanzani na Mkuu wa Chuo mwanzilishi;

Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Chuo;

Dkt. Adolf B. Rutayuga, Kaimu Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi;

Bw. John Mihayo Cheyo, Kamishna wa Bajeti Tanzania;

Mheshimiwa January S. Lugangika, Mkuu wa Wilaya;

Mheshimiwa Shabani Shekilindi, Mbunge Jimbo la Lushoto;

Mheshimiwa Kazimbaya Makwega, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Lushoto;

Viongozi wa Dini na Vyama vya Siasa;

Ndugu Wahadhiri wa Chuo na Watumishi wa Chuo;

Ndugu Wazazi na Walezi wa Wahitimu;

Ndugu Wahitimu na Wanachuo Wote;

Wageni Walikwa;

Ndugu wanahabari;

Mabibi na Mabwana.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema, kwa kutuweka hai na wenye afya njema na kwa kutuwezesha kujumuika pamoja wote katika sherehe ya mahafali ya 16 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto. Ninayo heshima na furaha kubwa kukukaribisha hapa Chuoni, wewe pamoja na wageni waalikwa wote katika mahafali haya ya 16. Karibuni sana.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kwa niaba ya Menejimenti na watumishi wote wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, ninachukua fursa hii kukushukuru sana kwa kukubali mwaliko wetu kuja kushiriki nasi katika Mahafali haya ya 16 ya chuo hiki kwani ninatambua ya kuwa hii ni mara yako ya kwanza tangu uteuliwe kuongoza Wizara ya Katiba na Sheria, kujumuika nasi katika chuo hiki. Ni ukweli usiofichika kuwa mbali na majukumu yako mengi bado umeona umuhimu wa kujumuika nasi kwenye shughuli hii muhimu ya Mahafali ya Chuo. Hii inadhihirisha namna ambavyo Wizara, kama mdau mkubwa wa utoaji haki, inavyojali shughuli za Chuo hiki.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, mahafali ni tukio kubwa linaloashiria utendaji kazi wa umakini kwa Taasisi, wanajumuiya na wahitimu ambao wametumia muda, rasilimali watu, fedha na juhudi stahiki katika kuifikia siku hii ya leo. Napenda kuwapongeza watu wote ambao kwa namna mbalimbali wamesaidia kutufikisha hapa tulipo.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, naomba kukufahamisha kwamba katika Mahafali haya ya 16, jumla ya wahitimu 344 watatunukiwa Stashahada na Astashahada ya Sheria. Kati yao, wahitimu wa Stashahada ya Sheria ni 208 ambapo kati yao kuna wanawake 117 sawa na asilimia 56 na wanaume 91 sawa na asilimia 44. Wahitimu wa Astashahada ya Sheria ni 135, ambapo kati yake wanawake ni 72 sawa na asilimia 53 na wanaume ni 64 sawa na asilimia 47.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, napenda pia kuchukua fursa hii kutoa taarifa kwamba, wahitimu wanaotunukiwa vyeti vyao leo walianza masomo yao hapa chuoni katika mwaka wa masomo 2014/15 kwa kozi ya Stashahada ya Sheria ambayo ni ya miaka miwili. Aidha, wahitimu wa kozi ya Astashahada ya Sheria walianza masomo yao ya mwaka mmoja katika mwaka wa masomo 2015/16.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, naomba nitoe mwelekeo wa Udahili kitakwimu kwa takribani miaka mitatu mfululizo.

MWAKA WA MASOMO

WALIOSAJILIWA KOZI YA STASHAHADA YA SHERIA

WALIOSAJILIWA KOZI YA ASTASHAHADA YA SHERIA

JUMLA

2014/2015

256

249

505

2015/2016

193

239

432

2016/2017

231

185

416

JUMLA

680

673

1,353

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, napenda pia kukufahamisha kwamba, katika mwaka wa masomo 2016/17, kama nilivyokwisha eleza, Chuo kimedahili jumla ya wanachuo wapya 416 kwa mchanganuo ufuatao; wanachuo 231 kwa kozi ya Stashahada ya Sheria na kati ya hao, wanaume ni 129 na wanawake ni 102. Kwa upande wa kozi ya Astashahada ya Sheria, Chuo kimedahili wanachuo 185. Kati yao, wanawake ni 101 na wanaume ni 84.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kwa mujibu wa takwimu nilizowasilisha hivi punde, zinaonesha kuwa hakuna ongezeko la udahili katika mwaka huu wa masomo ukilinganisha na mwaka wa masomo 2015/2016. Hii ni kutokana na changamoto za miundo mbinu ambazo Chuo kinakabiliana nazo. Changamoto hizo zinajumuisha:-

  • a)Ufinyu wa jengo la Maktaba ambalo halikidhi uwepo wa idadi kubwa ya wanachuo;
  • b)Ufinyu wa kumbi za mihadhara na malazi kutokana na kusuasua kwa utekelezaji kwa wakati, mipango ya upanuzi wa miundo mbinu ambayo unaathiriwa na upungufu wa fedha; na
  • c)Vyanzo vya maji safi na salama kwa mji mdogo wa Lushoto havitoshelezi na kutokidhi mahitaji ya ongezeko kubwa la wakazi wake pamoja na jumuiya ya chuo.

Lengo ni kujenga miundombinu inayokidhi mahitaji ili kukiwezesha Chuo kuwahudumia wanachuo kulingana na miundombinu iliyopo.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, nachukua nafasi hii kukufahamisha kwamba, kwa lengo la kuwajengea wanachuo wetu wapya uwezo wa kuhimili mafunzo yanayoendeshwa hapa chuoni, Chuo kimekuwa kikiandaa mafunzo maalumu ya kuwaandaa wanachuo wapya kwa kuwapa mafunzo ya mbinu za kujifunza kwa kipindi cha majuma mawili yakijumuisha namna ya kutumia Sheria mbalimbali ili kuwawezesha kujenga hoja. Kwa kipindi cha miaka mitatu sasa tangu mafunzo hayo yamekuwa yakitolewa, yameonesha kuwa ya manufaa makubwa katika kuwajengea wanafunzi uwezo wa kumudu masomo yao na namna ya kukabiliana na kazi za kitaaluma wanazopewa na wahadhiri.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, napenda pia kuchukua fursa hii kukujulisha kuwa katika jitihada za kuboresha utoaji wa Mafunzo ya Stashahada na Astashahada na vile vile katika lengo la kukijengea Chuo uwezo wa kutoa Mafunzo ya Kimahakama, Chuo kimeingia makubaliano ya ushirikiano na Taasisi zifuatazo:-

1.Taasisi ya Mafunzo ya ESAMI;

2.Chuo Kikuu Huria cha Tanzania;

3.Chuo cha Mafunzo ya Kimahakama cha Canada (National Judicial Institute);

4.Taasisi ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo (Law School of Tanzania);

5.Wakala wa Mafunzo kwa njia ya Mtandao (Tanzania Global Learning Agency);

6.Wakala wa Serikali Mtandao (eGovernment Agency).

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, naomba kuchukua fursa hii kuwapongeza wahitimu wote watakaotunukiwa Stashahada na Astashahada ya Sheria ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto leo. Hongereni sana.

Ni Matumaini yangu kwamba, kila mmoja wetu tuliopo hapa, ni mwenye furaha kwa namna moja au nyingine. Kwa upande wetu Chuo, furaha tuliyonayo inatokana na kazi kubwa ya kufundisha, kuongoza na kukijenga Chuo na kufikia mafanikio haya makubwa ambayo leo hii tunajivunia, likiwemo la kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu mzuri kwa program zote za Astashahada na Stas...