HOTUBA YA MWENYEKITI WA BARAZA LA UONGOZI WA CHUO, MHE. JAJI MSTAAFU WA MAHAKAMA YA RUFAA TANZANIA, JOHN A. MROSO, KWENYE SHEREHE YA MAHAFALI YA KUMI NA SITA YA CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA LUSHOTO

TAREHE 02 DESEMBA, 2016

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb), Waziri wa Katiba na Sheria;

Mheshimiwa Jaji Aishieri Sumari, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Moshi;

Mheshimiwa Jaji Imani Aboud, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Tanga;

Mheshimiwa Professor Sifuni Mchome, Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria;

Mheshimiwa Emilian E. Mushi, Jaji Mstaafu Mahakama Kuu ya Tanzani na Mkuu wa Chuo mwanzilishi;

Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Chuo;

Mheshimiwa Pamela Mazengo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga;

Dkt. Adolf B. Rutayuga, Kaimu Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi;

Bw. John Mihayo Cheyo, Kamishna wa Bajeti Tanzania;

Mheshimiwa January S. Lugangika, Mkuu wa Wilaya;

Mheshimiwa Shabani Shekilindi, Mbunge Jimbo la Lushoto;

Ndugu Wahadhiri wa Chuo na Watumishi wa Chuo;

Ndugu Wazazi na Walezi wa Wahitimu;

Ndugu Wahitimu na Wanachuo Wote;

Wageni Walikwa;

Ndugu wanahabari;

Mabibi na Mabwana.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kwa kutujalia afya njema leo hii na kutuwezesha kujumuika pamoja katika tukio hili kubwa na adhimu la Mahafali ya 16 ya Chuo chetu.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, tunafahamu fika kwamba una majukumu mengi na mazito ya Kitaifa yanayohitaji muda wako kila siku. Hata hivyo umeweza kutupa heshima kubwa na ya kipekee kwa kukubali mwaliko wetu kuwa Mgeni Rasmi katika Mahafali haya ya Kumi na Sita ya Chuo chetu. Kwetu sisi, hii ni heshima kubwa sana uliyotupa na tutaithamini sana.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, naomba niendelee kukiri kwamba ujio wako umeonesha ni jinsi gani wewe binafsi na Wizara ya Katiba na Sheria unayoiongoza, mnavyothamini elimu ya Sheria na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ambacho ni taasisi muhimu katika kuboresha shughuli za utoaji haki.

Ninaomba nichukue fursa hii, kwa niaba ya Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, kukukaribisha rasmi hapa chuoni. KARIBU SANA.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, ninaomba, kwa niaba ya Baraza la Uongozi wa Chuo, nichukue nafasi hii kukupongeza kwa kuteuliwa kwako kuiongoza Wizara ya Katiba na Sheria. Tunatambua uwepo wa changamoto kadhaa zinazokabili nchi yetu kwa sasa katika fani ya utoaji haki, hivyo tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu, aendelee kukujalia afya njema, hekima na weledi katika kuiongoza Wizara hii kufikia malengo yake ya haki sawa na kwa wakati.

Aidha, ninaomba nami kuungana na Mkuu wa Chuo, kuwakaribisha viongozi mbalimbali, wageni waalikwa, wazazi, ndugu na marafiki wote, kushiriki nasi katika mahafali haya. Kwetu sisi, hii ni heshima kubwa mliyotupa kwa vile mmeacha kazi zenu nyingi na kuja kujumuika nasi. KARIBU SANA.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, nachukua fursa hii kukufahamisha kwamba, Chuo kimepata mafanikio mbalimbali tangu kuanzishwa kwake katika nyanja za taaluma. Mafanikio ya kitaaluma yaliyopatikana katika kipindi cha miaka kumi na sita tangu Chuo kianzishwe hadi sasa, yanatokana na maamuzi yenye weledi, busara, hekima na uthubutu wa viongozi mbalimbali wa Baraza la Uongozi wa Chuo waliopita kwa kusimamia vyema Mipango ya Chuo na kusimamia vyema utekelezaji wa sera mbalimbali zilizowezesha Chuo kufikia malengo yake. Viongozi hao wa Baraza la Uongozi wa Chuo walishirikiana bega kwa bega na Menejimenti ya Chuo katika kufanikisha malengo ya Chuo tangu kilipoanzishwa.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kuhusu maendeleo ya kitaaluma, napenda kukufahamisha kuwa wahitimu wetu wamekuwa wakiajiriwa kama maafisa kumbukumbu wasaidizi na makarani katika Mahakama ya Tanzania na kwingineko hapa Tanzania kama vile Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pia Ofisi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini, kama Afisa Usajili. Hii inatokana na ubora wa elimu inayotolewa hapa chuoni.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Katika juhudi za utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Chuo wa kukijengea uwezo wa Rasilimali watu kwa ajili ya utoaji wa elimu bora hapa chuoni, Chuo kwa sasa kina jumla ya wanataaluma ishirini na tano (25) ambao katika kipindi cha miaka kumi na sita iliyopita wameendelezwa kitaaluma kwa kupatiwa Kozi ndefu na fupi ili kuwajengea uwezo zaidi kitaaluma katika maeneo yao ya Ubobezi, na hivyo kukiwezesha Chuo kupata mafanikio ambayo leo hii kinajivunia.

Miongoni mwa wanataaluma hao, wanataaluma wawili (2) wamemaliza shahada zao za uzamivu na wanaendelea na majukumu yao mbalimbali, wanataaluma wengine watatu (3) kwa sasa wapo kwenye hatua mbalimbali za masomo ya Shahada ya Uzamivu katika maeneo yao ya Ubobezi.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, napenda kukuhakikishia kwamba idadi ya wahadhiri waliopo Chuoni kwa sasa inajitosheleza ukilinganisha na idadi ya wanachuo waliopo.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, katika moja ya mafanikio yake kitaaluma, Chuo kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania, kimeendelea kuitumia vema Kurugenzi ya Mafunzo Endelevu ya Kimahakama iliyopo chuoni. Ili kuimarisha na kuongeza ufanisi katika Kurugenzi hii, Mahakama ya Tanzania imewahamishia Chuoni, Mahakimu Waandamizi watatu (3). Kurugenzi hii kwa kushirikiana na Kurugenzi ya Mafunzo ya Mahakama, imeendelea kuratibu na kuendesha mafunzo ya muda mfupi, yaani Semina; Warsha, na Kozi fupi za kuwaongezea weledi watumishi wa ngazi zote wa Mahakama ya Tanzania na Taasisi nyingine.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kuanzia mwezi Novemba 2014 hadi mwezi Novemba, 2016 Chuo kwa kushirikiana na Kurugenzi ya Mafunzo ya Mahakama Tanzania kimefanikiwa kuendesha semina, kozi, warsha fupi zifuatazo kwa watumishi wa kada mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania. Baadhi ya kozi na semina zilizoendeshwa ni kama ifuatavyo:-

(i)Semina ya Mahakimu kuhusu uandishi wa Hukumu iliyofanyika hapa Chuoni kuanzia tarehe 26 hadi 28 Novemba, 2014 na semina kama hiyo kwa Majaji iliyofanyika tarehe 01 hadi 03 Desemba 2014.

(ii)Semina ya Mahakimu Wakazi kuhusu Uendeshaji na Usimamizi wa Mashauri iliyofanyika hapa Chuoni kuanzia tarehe 23 hadi 25 Februari, 2015.

(iii)Kozi ya uendeshaji wa mashauri ya upatikanaji wa mali zilizopatikana kwa uhalifu (Stolen Asset Recovery) kwa mahakimu ishirini na tano (25) iliyofanyika hapa Chuoni kuanzia tarehe 18 hadi 22 Mei, 2015 kwa kuwatumia wawezeshaji wa ndani (Majaji na Mahakimu) na nje ya nchi hususan Uingereza, Uholanzi na Kenya ili kuwawezesha Mahakimu kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazohusiana na kesi hizo na kuzitolea maamuzi ipasavyo kwa mujibu wa sheria.

(iv)Semina inayohusu TEHAMA, mwezi Februari, 2016.

(v)Semina ya Mahakimu na Wasajili, mwezi Septemba, 2016

(vi)Mafunzo kwa Wakufunzi wa Haki za Binadamu, kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa kushirikiana na Chama cha Majaji Wanawake (TAWJA) na UNWomen kuanzia tarehe 10/10/2016 hadi 14/10/2016.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo, kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania, Chuo kimeratibu na kuendesha mafunzo elekezi ya waheshimiwa Majaji wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Mafunzo hayo elekezi yalifanyika hapa Chuoni kwa kipindi cha wiki tatu mfululizo na kwamba mwaka 2014 Majaji ishirini (20) walishiriki mafunzo hayo. Kwa mwaka...